Sunday, February 20, 2011

Mpango wa MWAKEM: “Usiwe Jibu rahisi kwa tatizo kubwa !”

Dec, 16, 2010 taasisi ya uwezo Tanzania ilitangaza matokeo ya utafiti wake kuhusu uwezo wa watoto kusoma na kuandika nchini Tanzania. Katika utafiti huo, imebainika kuwa idadi kubwa ya watoto nchini hawawezi kufaulu majaribio kwa kiwango kilichotarajiwa. Matokeo ambayo kimsingi yanatoa wito wa kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika kila somo.


Kwa muda mrefu sasa, jamii imekuwa ikiwatupia mzigo mkubwa wa lawama walimu pindi ufaulu wa wanafunzi unapo kuwa duni. Kimantiki lawama hizo zinaweza kuwa na mashiko. Hii inatokana na ukweli kuwa ubora wa elimu itolewayo unategemea sana uwepo wa walimu wenye sifa,vifaa vya kufundishia na kujifunzia, mitaala thabiti na thahili,ushirikiano wa walimu, wanafunzi, wazazi,wadau wa elimu na tathmini sahii ya mtaala inayokubalika.

Kwa kutambua kuwa ubora wa walimu ni kigezo muhimu cha msingi katika kuinua ubora wa elimu, Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ili kukidhi mahitaji katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya sekta ya elimu (ESPP)ambao ilihusisha mipango kabambe ya MMEM na MMES iliandaa mkakati wa menejimenti na maendeleo ya walimu MMEMWA ili kuimarisha ubora wa elimu ya ualimu. Hii ilitokana na ukweli kuwa mafanikio ya mipango yote miwili MMEM na MMES litegemea sana upatikanaji wa walimu.

Aidha, kwa kutambua kuwa mafunzo ya walimu kazini ni nyenzo kuu ya kufanikisha ubora wa ufundishwaji na ujifunzaji darasani.Serikali imeamua kuimarisha programu za mafunzo kazini kwa walimu .Kuanzia Julai ,2010, wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ilianza kutekeleza mkakati wa mafunzo kazini kwa walimu wa shule za msingi ngazi ya shule-MWAKEM kwa lengo la kuinua ubora wa walimu wa shule za msingi katika kufundisha elimu ya awali na msingi kwa ufanisi.

Ni dhahiri kuwa ikiwa mpango huu utaratibiwa na kusimamiwa vema walimu watapata kujifunza mambo mapya kama vile mabadiliko ya mitaala, dhana na nadharia za ufundishaji na ujifunzaji na hivyo kuweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko katika elimu kila wakati.

Kwa mujibu wa mwongozo wa usimamizi na utekelezajimwam MWAKEM uliotolewa novemba 2010,usimamizi na uendeshaji wa mafunzo kazini kwa walimu wa shule za msingi ngazi ya shule umeelekezwa vizuri sana.Aidha,watendaji wakuu katika utekelezaji huo na majukumu yao katika kila ngazi wameainishwa vema.Na kwa lengo la kuwa na mafunzo yenye ufanisi na endelevu kwa walimu mafunzo hayo yameandaliwa kutolewa kwa kushishikiana na halmashauri za wilaya.

Nashawishika kuuona mpango wa MWAKEM kuwa ni jibu rahisi kwa tatizo kubwa kwa sababu kuu mbili; mosi ni uzoefu unaotokana na utekelezaji wa mipango iliyotangulia na pili ni pengo kubwa lililopo kati ya ukweli wa hali ya elimu yetu na jitihada za mantiki tunayotumia ili kuuona ukweli huo katika kutathimini na kuinua ubora wa elimu nchini.

Utekelezaji wa mipango mingi ya maendeleo ya elimu iliyotangulia umekuwa na changamoto nyingi sana.Mfano mzuri katika kuelezea hili ni mpango wa mafunzo kazini kwa walimu wa daraja la tatu B/C-A mpango uliokuwa maarufu sana kwa jina la “moduli”. Utekelezaji wa mpango huo ulikumbana na changamoto nyingi sana.Kubwa miongoni mwa changamoto hizo ilikuwa ni utayari wa walimu tarajiwa kujiendeleza kuwa mdogo na halmashauri nyingi kutotenga fungu kwa ajili ya mafunzo kabilishi na yale ya ana kwa ana kati ya wakufunzi na walimu ili kutathimini maendeleo ya walimu katika kujifunzaji. Kwa mujibu wa mwongozo wa utekelezaji wa MWAKEM kila halmashauri imeelekezwa kutenga pesa kiasi cha tsh elfu arobaini [40,000/=] kwa kila mwalimu kwa ajli ya mafunzo hayo kila mwaka katika bajeti yake.Uzoefu unaonyesha kuwa halmashauri nyingi kipaumbele chao huwa sio maendeleo ya taaluma ya walimu na ndio maana mafungu hayo huwa hayapo na ikitokea yakatengwa huwa yanatumika kwa shughuli nyingine tofauti na malengo tarajiwa.Tatizo linaloonekana kuwa sugu.

Nimelazimika kutolea mfano mpango wa C/B-A na MWAKEM kwa kuwa wahusika wakuu katika utekelezaji wake ni wale wale na mfumo wa uendeshaji wake hauna tofauti na ule wa C/B-A ambao mafunzo yake yalitolewa kwa njia ya masafa kupitia moduli.

Sababu nyingine inayonifanya kuuona mpango huu ni jibu rahisi kwa taizo kubwa kama nilivyodokeza hapo awali ni pengo kubwa lililopo kati ya ukweli halisi wa hali ya elimu yetu na jitihada za mantiki tunayotumia ili kuuona ukweli huo katika kutathimini na kuinua ubora wa elimu nchini.Kwa mfano,ni ukweli usiopingika kuwa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji darasani unategemea sana umahiri wa mwalimu.Ni udhaifu mkubwa ikiwa tutakuwa tunazungumzia mpango wa kumpata mwalimu “mahiri” pasipo kueleza njia na vigezo tutavyotumia katika kumpata na jinsi ya kumfanya auishi umahiri wake.

Napenda kuwakumbusha wadau na wanaharakati wa elimu kuwa ubora wa elimu ni zaidi ya kuwa na mwalimu “mahiri” kwani hutegemea sana uwepo wa mitaala thabiti na dhahiri,uwepo wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, walimu wenye sifa,miundombinu inayovutia ufundishaji na ujifunzaji na ushirikiano wa wazazi,walimu,wanafunzi na wadau wote wa elimu.

Aidha napenda kuwakumbusha pia kuwa pamoja na ukweli kuwa elimu yetu inachangamoto nyingi,bado mafunzo kazini kwa walimu ni ya lazima na yanayopaswa kuwa endelevu.Ikiwa mifumo ya uendeshaji na usimamizi itaimarishwa ni dhahiri kuwa kiwango cha ufundishaji wa walimu wetu kitaimarika na hivyo lengo la taifa la upatikanaji wa elimu bora kwa wote litafanikiwa.