Saturday, January 16, 2010

CWT yavuna zaidi ya Tshs.3,550,092,000.00/=za walimu isivyohalali kila mwaka!!


Awali ya yote namshukuru Muumba kwa kutuwezesha kuifikia siku ya leo ambapo saa chache zijazo tutauanza mwaka mpya wa 2010.Aidha napenda pia kuchukua nafsi hii kuwashukuru wasomaji wa makala zangu hasa wale wanaoperuzi gazeti langu tando la www.pengotz. blogspot. com. Pamoja na ukweli kuwa kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikichangia makala katika majukwaa mbalimbali kuhusu walimu na CWT,leo nimeamua kufunga mwaka na makala nyingine kuhusu CWT.Kifupi naweza kusema kuwa makala hii ni mjumuisho wa makala na michango yangu iliyotangulia kuhusu CWT.

CWT ni trade union ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuw walimu hapa nchini wanapata stahili zao kwa wakati.Pamoja na ukweli kuwa CWT imejitahidi kwa kiasi kikubwa sana katika kutekeleza wajibu huo bado chama hicho kina mapungufu kadhaa ya kimuundo na kiutendaji. Katika makala hii ya kuhitimisha mwaka ningependa kujadili kuhusu swala la uanachama na makato ya ada ya uanachama kama ambavyo nimekuwa nikifanya hapo nyuma.

Kuhusu swala Uanachama,katiba ya CWT inasema kuwa kuna aina tatu za wanachama wa chama hicho.Aina ya kwanza ni wanachama wa heshima ambao hupewa uanachama kutokana na mchango wao kwa chama,Aina ya pili ni uanachama wa hiari na ile ya mwisho ni wanachama wa halisi ambao wanatoa ada ya uanachama kila mwezi.Upungufu uliopo katika kipengele cha wanachama ni katiba kutotoa maelezo ya kutosha kuonyesha namna ya upatikanaji wa hao wanachama halisi. Jambo jingine ninaloliona kuwa ni upungufu/udhaifu ni kuhusu ada ya uanachama.Tangu nimeifahamu CWT haijawahi kuwa na kiwango sawa cha makato ya ada ya uanachama kwa wanachama wake.CWT imekuwa ikikata 2% ya mshahara wa kila mwalimu kila mwezi kama ada ya uanachama. Kwa maswala hayo mawili ya uanachama na makato ya ada kwa asilimia 2% ya mshahara wa mwalimu kila mwezi kwangu naliona kuwa ni tatizo kubwa ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka kadri inavyowezekana. Wakongwe katika sekta ya elimu wanashuhudia kuwa enzi zao walikuwa wakijaza fomu maalumu kwa ajili ya kujiunga na CWT na kila mmoja alipewa nambari ya uanachama pamoja na kadi ya chama.Jambo la kusikitisha hali hiyo siku hizi haipo kwani kila anayeitwa mwalimu na kufundisha shule au chuo cha serikali basi mara moja anaanza kukatwa ada ya uanachama katika mshahara wake pasipo ridhaa yake huku wale walio katika sekta binafsi wakiwekwa kando.! Aidha, swala la makato ya ada ya uanachama kwa asilimia ya mshahara wa mtu ni aina nyingine ya ufedhuli usioweza kuvumulika wanaofanyiwa walimu hapa nchini.CWT inavuna mamilioni ya pesa za walimu isivyo halali kila mwezi kwa mtindo huo na kutufanya tujiulize hivi CWT-kwa-maslahi- ya-nani?walimu, serikali, AU Viongozi wake?

Nathubutu kusema kuwa CWT inavuna pesa za walimu isivyohalali kila mwezi kutokana na ukweli kuwa kwa mujibu wa sheria zilizopo hawana mamlaka ya kuchukua ada ya uanachama kwa asilimia ya mshahara wa mtumishi.Nasema hayo kwa kuwa nimelazimika katika kuutafuta ukweli kudurusu sheria mabalimbali tangu ile ya mwaka 1961,"The organisation of Tanzania Trade Union Act,1961,[Act no. 20/91],the trade Union(Revocation of special powers) Act,1962,The Trade Union ordiance Act,1962,"The Trade Unions and Trade Disputes (Miscellaneous Provision)Act, 1964 [Act No. 64/64] hadi hii ya sasa iliyofanyiwa marekebisho 2006 "The Trade Union Act,1998 sijaona mahali ambapo wamepewa mamlaka ya aina hiyo isipokuwa kwa sheria ya "Employment and Labour Relations Act,2004 part 4 ndiyo inayotoa maelekezo ya kitu gani kifanyike baada ya mwajiriwa kuridhia mbele ya mashahidi kuhusu makato husika [Sio kwa %] ya mshahara wake kwenda katika trade union husika. Kwa mantiki hiyo,CWT imekuwa ikuvuna zaidi ya Tshs.3,550,092,000.00/=i kila mwaka tangu mwaka 2002 hadi sasa kutoka kwa walimu pasipo ridhaa yao.Hesabu hiyo hapo juu ni ndogo sana nayo inatokana na walimu waliopatikana kutokana na utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya sekta ya Elimu chini ya programu mbili za MMEM [2002-2006] Ambao uliiwezesha serikali kuajiri walimu wapya 45,796 wa shule za msingi wakati kupitia SEDP [2004-2009] walimu 38,730 wa ngazi ya shahada na stashahada wameajiliwa na kufanya jumla ya walimu wapya walioajiriwa katika sekta ya elimu kati ya mwaka 2002 na 2009 kufikia 84,526.Walimu hao wote hawajawahi kujaza fomu za kujiunga na chama wala kuridhia makato ya ada ya uanachama wa 2% ya mshahara wao. Ikiwa walimu hao kila mmoja atakuwa anakatwa wastani wa Tshs.3500/- kila mwezi,kwa mwaka mmoja CWT inavuna isivyohalali Tshs. 3,550,092,000. 00/=

Nawaandikia makala hii walimu kwa kuwa naamini kuwa walimu ni watu waelewa,wenye hekima na wanaoamini katika kile wanachokiamini kuwa ni sahihi.Nao watatumia busara zao katika kulitathimini jambo hili na kulitafutia ufumbuzi. Aidha ,nawaandikia watanzania kwa kuwa naamini kuwa wao ni watu makini,wachambuzi na wenye busara ambao siku zote hawapo tayari kuona uonevu ukifanywa katika jamii yao.Nao watakuwa tayari kuwaunga mkono watu hawa waliopewa jukumu kubwa la malezi ya watoto wetu katika mazingira magumu huku wakinyimwa haki zao za msingi za kiutumishi. Ninamwandikia katibu mkuu -Hazina na waajiri wote wa walimu [Katibu mkuu,Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi na Wakurugenzi wa halimashauri zote za wilaya] ili watambue kuwa makato wanayoyafanya ya 2% ya mshahara wa kila mwalimu kama ada ya uanachama kwenda CWT sio halali na wanapaswa kusitisha na kuchukua hatua haraka iwezekanavyo. CWT nao wanapaswa kujipeleleza na kuunda chama imara upya ambacho sio tu kitakuwa kikisimamia na kuratibu upatikanaji wa haki na maslahi ya walimu bali kuhakikisha kuwa kinasimamia ipasavyo maendeleo ya Taaluma ya Ualimu hapa nchini.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

Nawatakia Kila lakheri katika mwaka Mpya wa 2010.