Nimeanza makala hii kwa maelezo hayo katika kuutafakari msamiati wa “Mtoto wa Mkulima” ili niweze kuonyesha pengo kubwa lililopo kati ya ukweli wa maisha yetu na jitihada za mantiki tunayotumia ili kuuona ukweli huo.
Msamiati wa “Mtoto wa Mkulima” umeshika kasi ya ajabu sana katika siku za hivi karibuni.Ulipoanza kutumika msamiati huu,watumiaji wake walikuwa wakimaanisha kweli wao ni watoto wa wakulima,watu safi,wenye kuenenda katika mapito safi na waliotayari kupigania maslahi ya wengi.Kutokana na hali hiyo,ndipo wafuasi lukuki wakajitokeza mstari wa mbele katika kuunadi msamiati huo.
Jumuia ya wanachuo wa chuo kikuu cha Dar es salaam ni moja ya maeneo ambayo msamiati wa mtoto wa mkulima umeshika kasi ya ajabu!!!!Wanazuoni kadha wa kadha wakijipambanua kama wanaharakati wamekuwa wakijinadi kama watoto wa wakulima ilihali kihalisia sio kweli-hawako hivyo hata kidogo!! Wamekuwa wakijitokeza mbele ya hadhira mikono nyuma wakiendeleza kile wanazuoni wanachokiita “Vuguvugu la Umajumuni” katika kupinga mifumo dhalimu inayotufanya kuafiki kile tusicho amini.Jambo la kusikitisha ni pale wanapopewa mamlaka/madaraka ya kuwaongoza wenzao ghafla hunaswa katika mikoba ya ya uchawi wa “Giningi” na kusahau kabisa misingi ya harakati zao na kisomo chao kilichowapa nafasi ya kuwa pale walipo. Wanaishia kufanya kinyume na kabisa matarajio ya watu na kuwaacha “ watoto wa wakulima” halisi wakiishi na tamaa zao katika hali ya kukata tamaa!!!?
Binafsi sishangai hali hii kutokea.Sishangai kwa kuwa ni hali niliyoitegemea.Ni hali iliyotegemewa kwa kuwa tangu enzi za uhuru wan chi hii waasisi wake walisema wazi kabisa kuwa hii ni nchi ya wakulima na wafanyakazi.Baada ya wakulima kujipambambanua kuwa wao ni watu safi na wapiganaji katika ujenzi wa “Dunia bora kwa wote”, watoto wa wafanyakazi hasa wale wenye kipato kilichotukuka na kubatizwa majina yenye kuchukiza!? Hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kuingia katika mduara na kujifanya nao ni wachezaji wa mdundo wa “Utenzi wa watoto wa wakulima”.Watoto wa wakulima wakadanganyika na kufikiri ni wenzao.Wanaposhituka,tayari wachezaji wakuu wa utenzi huo ni wale wale “waliotengwa”-hatimaye wametekwa nyara!!.Ishara ya hali hiyo ni matokeo ya utendaji wa viongo wetu ambao awali tulidhani ni wenzetu???!!!
Wanazuoni!!!! Ikiwa bado tunaamini katika misingi ya waasisi wa taifa letu ya kuwa hii ni nchi ya wakulima na wafanyakazi.Basi huu ni wakati wetu muafaka kudurusu upya mantiki ya msamiati huu wa “ mtoto wa mkulima” ili kuupatia maana stahili katika wakati stahili. Katika kufanya hivyo ni budi tukajikita vema katika kuangalia vigezo tunavyovitumia kutambua motto wa mkulima au vinginevyo kama haja hiyo ipo na mantiki tunayoitumia katika kuwagawa “ watoto wa watanzania” katika madaraja/makundi hayo.
Binafsi, nafikiri huu ni wakati muafaka wa kuzungumzia “uzalendo” . Tuwazungumzie watoto wa wazalendo wa Tanzania [Wakulima: wadodo,wakati & wakubwa Na wafanyakazi: wa kima cha chini,kati na juu].Ikiwa msamiati wa “mtoto wa mkulima” tumekuwa tukilitumia kumpambambanua mtoto wa Mtanzania mwenye kipato cha chini basi hilo ni kosa kubwa ambalo hatuna budi kuacha kuendelea kulifanya haraka iwezekanavyo kwa kuwa sio kweli kuwa kila mtoto wa mkulima anatoka katika familia duni.Aidha,ikiwa msamiati huo tunautumia katka kuwapambanua “ wapiganaji” au wanaharakati wa vuguvugu la umajumuni basi huu ni wakati muafaka wa kutafuta msamiati sahihi baada ya msamiati wa “ mtoto wa mkulima kutekwa nyara!!!!.Hii ni nchi ya wakulima na wafanyakazi.
Kazi ya mja kunena
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania!!!!!