Sunday, March 30, 2008

Upimaji huu katika Elimu hauna tija

Sasa naanza kuiamini ndoto yangu niliyowahi kuota zamani kidogo.Ndoto hiyo ilihusu kuondolewa/kufutwa kwa mtihani wa darasa la nne, kidato cha pili na kubali aina ya upimaji wa wanafunzi katika elimu ya juu hapa nchini.

Imani yangu kuwa ndoto yangu inaweza kutimia inatokana na kauli ya Amiri jeshi mkuu ambaye pia ndiye Rais wa Jamhuri yetu aliyoitoa katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa Elimu wa mwaka huu uliofanyika Ubungo Plaza mwanzoni mwa mwezi huu.Katika ufunguzi wa mkutano huo,Rais alitoa changamoto kwa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kuitaka kuangalia upya utaratibu wa mtihani wa darasa la nne na umaana wake.

Nisingependa kujiumiza kichwa kutafakari msingi wa kauli hiyo ya JK ikiwa ni ya kisiasa au kitaalam kwani kihalisia swala hilo halihitaji mtu kuwa na PhD ya Ualimu kulibaini.

Mantiki ya kuwepo au kutokuwepo kwa mtihani wa darasa la nne na ule wa kidato cha pili ni swala ambalo nimekuwa nikilizungumzia mara nyingi sana na watu ninaokutana nao na kufanya nao kazi hasa katika warsha na semina ninazohudhuria kwa muda mrefu.

Pamoja naukweli kuwa nimefarijika sana kuona kuwa mamlaka imetambua upungufu uliopo katika utekelezaji wa mfumo wetu wa elimu,nasikitika kuona kuwa walimu na waelimuisha walimu tulikuwa kimya hadi wanasiasa wanapotuaibisha majukwaani kwa kutukumbusha wajibu wetu wa “Kufikiri kwa kina kuhusu mustakabali wa Elimu na maendeleo yake hapa nchini”.

Upimaji kwa kutumia mitihani ya taifa kwa darasa la nne na kidato cha pili hauna tija kwa kuwa mitihani hiyo hupelekea hukumu ya kielimu kwa wanafunzi ambao kasi na wepesi wao katika kujifunza ni mdogo,bila kuzingatia mambo yote yanayomzunguka katika kuipata Elimu hiyo.Jambo lililopelekea/sababisha elimu yetu kuwa ya kukariri/kujiandaa kushinda mitihani na kuliacha kundi kubwa la vijana wetu wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa taifa likipotea.Bonyeza hapa usome zaidi kuhusu swala hili

Ninapotafakari ni kwa kiasi gani taifa limeingia hasara kwa kuwapoteza vijana ambao wangeweza kutoa mchango kwa taifa letu baada ya kuchujwa na mitihani hiyo namkumbuka rafiki yangu mmoja ambaye nilipata kusoma nae shule ya msingiHuyu sio mwingine bali ni Tanzania one! {Waliohitimu meta sekondari au Mzumbe kati ya 1999-2002 wanaweza kumkumbuka}.Jamaa huyu tangu tulipoanza darasa la kwanza hakuwahi kuwemo hata katika wanafunzi 50 bora.Kwa bahati wakati huo mtihani wa darasa la nne ulikuwa umefutwa hivyo alitubeba hadi darasa la saba.

Kwa kuwa hakuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari za serikalikama wengi tulivyokuwa tumetarajia,alilazimika kutafuta shule ya Private.Alichukua fomu na kufanya usaili katika shule za Airwing,JKT Yombo Tech,Kiabasila na Makongo.Huko kote hakupata nafasi.Baada ya kuona muda unakwisha,baba yake ambaye kwa wakati huo alikuwa akiishi na kufanya kazi Mbeya aliamua kumuita ili akafanya masomo ya ufundi huko.Haijulikani nini kilitokea.Lakini tunachofahamu muda wa usaili Meta ulikuwa umeshapita nae hakufanya usaili hapo ila shule ilipofunguliwa alivaa sare na kuingia darasani.Miaka miwili na nusu ya kwanza yote hakuonyesha mwelekeo lakini alibadilika ghafla mhula wa pili wa kidato cha tatu na mwisho wa siku mtihani wa taifa wa kidato cha nne alipata daraja la kwanza pointi 09 na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano & sita shule ya sekondari Mzumbe.Alipewa jina la Tanzania one baada ya kuwa anaongoza karibu katika kila mtihani.Na katika mtihani wa Taifa wa kidato cha sita alidhihirisha hilo kwa kuwa mwanafunzi wa kwanza aliyefaulu vizuri zaidi kitaifa.

Huyu niliyemzungumzia hapa ni mmoja tu kati ya maelfu ya wanafunzi wenye uelewa wa pole pole ambao ukuaji wao kiakili ni wa taratibu sana ambao tumewapoteza kwa kuwa tu eti wamefeli mtihani wa darasa la nne au kidato cha pili.

Tanzania one alihitaji miaka 11 kuubainishia ulimwengu kuwa kuwa yeye nii exceptional kiakili {Gifted!?}.Ikiwa angepita katika zama hizi za mitihani ya std 4 na kidato cha 2 hakika jamaa angeishia kulima kokoa na kuuza maparachichi Mwanjelwa kama sio peremende mtaani.

Tunawahukumu wanafunzi wetu kila wanapofika darasa la nne na kidato cha pili kwa kuendelea na darasa linalofuata,kukariri/rudia darasa au kutoendelea kabisa na elimu[{Ugaidi!?}] kinyume kabisa na matarajio ya mfumo wetu wa elimu [2:7:4;2:3+] ambao unataka mtu asome na kufanyiwa upimaji tamati anapofikia mwisho wa kozi ,yaani std 7 au form 4.

Wanazuoni na wadau wote wa Elimu,Dhambi ya kutengeneza vibaka na wazururaji {kuwahukumu kwa kuwanyima fulsa ya kuendelea na masomo} tofauti na malengo ya elimu nchini tumeifanya kwa muda mrefu sasa.Ikiwa tunaikubali na kuiungama dhambi hii,ni vema sasa tukaamua kwa dhati kutoendelea kuitenda kwa kufanya maboresho yanayotakiwa.

Walimu, waelimisha walimu na wadau wote wa elimu kwa ujumla tunapaswa kuliona hili.Kwa mtazamo wangu swala la kuondolewa kwa mitihani hiyo halihitaji mjadala wala utafiti kwani dhamira/kusudio la la mfumo wetu wa elimu ni kumfanya kila anayeanza shule ya msingi au sekondari amalize sio kuishia njiani.

Labda kwa kumalizia napenda kuwakumbusha wenzangu kuwa Mheshimiwa J.K ameliona swala la mtihani wa std 4 na kidato cha 2.Sisi kama Educational Practitioners tunapaswa kwenda mbele zaidi katika kufikiri kwetu na kuangalia mfano ikiwa upimaji tamati unampima mwanafunzi katika nyanja zote tatu?( yaani nyanja ya maarifa/ufahamu,Uelekeo na Stadi) Katika hili kwangu naona kunatatizo kubwa ambalo linahitaji mjadala mpana na wa kina.Hata hivyo si vibaya nikidokeza kuwa hatuna budi kuiga kutoka kwa wengine mfano Afrika ya kusini ambao wanampatia credit mwanafunzi kadri anavyopanda darasa na inapotokea akafeli kabla ya kumaliza kozi wanamtambua(Certify) kwa kuonyesha kiwango cha darasa alichofikia .Tofauti na sisis ambapo mtu anayefanya kozi ya miaka mitano(5) chuo kikuu akishikwa 4th year hakuna anayemtambua kuwa aliwahi kufika chuo kikuu.Poleni watu mnaofanya MD.

Wednesday, March 5, 2008

Kilio cha Walimu:Ngoma isiyo na wachezaji?

Nini kikubwa mno unachoweza kututendea leo ambacho

bado hatujajitenda wenyewe?

Utatuambia nini leo ambacho bado

hatujajidanganya nacho?


Huwezi kujua ni miaka mingapi

tumezililia hadi tukaziangulia kicheko

njozi zetu zilizosambaratika na kubaki

vipande vipande.


Ndiyo

Tumeazimia kuyalazimisha matumaini

yetu yaliyokwisha potea kuwa njozi

thabiti kuliko unavyoweza kufikiri:

itangaze ukombozo wetu uliopatikana kwa

uchungu:

Kwa hiyo wala usituulize tunajishughulisha

na nini safari hii:

Mwenye ndoto haisahau hata

ijapokatishwa.

Nawe hutasalimika na hicho

tutakachokifanya.

Kutokana na vipande vya maisha yetu.



Nimeanza mada hii kwa utenzi huo wa mwanazuoni,malenga na mwanaharakati Prof.Abena Busia kwa makusudi ili kujikumbusha na kuikumbusha jamii kuhusu harakati za walimu kutafuta na kudai haki wanazostahili kutoka kwa waajiri wao(Katibu mkuu wizara ya Elimu na Wakurugenzi wa wilaya)


Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu sana harakati zinazofanywa na CWT kwa muda mrefu.Hii ni kutokana na ukweli kuwa siku zote huwa najitahidi sana kujustfy wazo langu nililowahi kulitoa hapo awali kuwa CWT sio chama cha kitaaluma(Rejea makala yangu kuhusu CWT na mustakabali wa Elimu nchini)


Ninaporejelea harakati za CWT hasa za viongozi wa ngazi za juu katika chama hicho,nafarijika kutambua kuwa walimu sasa wameutambua unyonge wao na sasa wanaazimia kuukana kama katiba ya chama hicho inavyoleleza katika sehemu ya utangulizi:

“KWA KUWA mwalimu ni kama raia mwingine yeyote nchini

ana haki ya kupata huduma bora za kijamii,kiuchumi

na kimaslahi kama vile afya,chakula,malazi,usafiri na

Huduma nyingine za kijamii.


Kwa hiyo BASI:Sisi walimu wote kwa pamoja tunaazimia

kuungana na kuunda chama chetu kitakachohakikisha kuwa

walimu wote tunatekeleza wajibu wetu na kupata

haki zote tunazostahili kutoka kwa waajiri wetu”


Nimeshawishika kuandika makala hii kutokana na matokeo ya kikao cha pamoja kati ya mawaziri wa TAMISEMI,Elimu,Menejimenti ya Utumishi wa umma na viongozi wa chama cha walimu kilichofanyika Febr. 22 mwaka huu chini ya waziri mkuu ambapo ilikubalika kuwa serikali itawalipa walimu madeni yao yote ifikapo mwezi huu.


Walimu,kwa hakika tuna kila sababu ya kuishinikiza serikali kupandisha mishahara yetu na kutulipa madai yetu mengine kama vile posho za kujikimu,malimbikizo ya mishahara na likizo.Hatuna sababu ya kuchuuzwa na matamshi yasiyomaanisha utatuzi wa matatizo yanayotusonga katika utekelezaji wa wajibu wetu-ndio maana Prof.Abena anatukumbusha kuwa”Utatuambia nini leo ambalo bado hatujajidanganya nacho? Je, ni miaka mingapi tumezililia shatili zetu hadi tukaziangulia kicheko?Ni matumaini yangu kuwa CWT na walimu wote kwa ujumla tumeazimia kwa dhati kuyalazimisha matumaini yetu yaliyokwisha potea kuwa njozi thabiti kuliko mtu yeyote anavyoweza kufikiri.Serikali inapaswa kutambua kuwa mwenye ndoto haisahau hata ijapokatishwa,nayo haitasalimika na kile tutachokifanya.


CWT na walimu kwa ujumla tunachangamoto kubwa katika kuhakikisha tunapata stahili zetu kutoka kwa waajiri wetu.Changamoto ya kwanza ni katika hulka ya itikadi na ya pili iko katika mikanganyiko yetu ya kiuharakati katika jumuia yetu bila kutambua kwa kina kile kinachocho tuunganisha na mipaka yake.

Kujielewa kwa namna ya kutuwezesha kubainisha na kutetete msimamo wetu ni changamoto nyingine tuliyonayo.Tunao wajibu wa kuwa wanafunzi wakati wote tukichambua bila kukoma hali ya walimu na jamii yetu katika enzi hizi za utandawazi ili kujifahamisha njia zinazotumika katika kutunyima stahili zetu na jinsi zinavyobadilika badilika.


Labda kwa kumalizi tu,niwakumbushe walimu kuwa silaha ya mwisho ya kila mfanyakazi Duniani ni kugoma pale anapoona hapati haki zake.Hatua hii ya wafanyakazi hufikiwa baada ya mwajiri kukaidi kusikiliza kilio chao kwa muda mrefu.


Alamsiki!