Sunday, February 20, 2011

Mitaala yetu na hatma ya Elimu Tanzania.

Utekelezaji wa shughuli mbalimbali za serikali huongozwa na sear na kusimamiwa na sheria zilizoundwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa katika kiwango kilichotegemewa.Tangu uhuru,sekta ya elimu hapa nchini imeongozwa na sera mbili ambazo ni sera ya elimu ya kujitegemea na sera ya elimu na mafunzo ya 1995.

 Ujio wa sera ya elimu na mafunzo 1995 ilikuwa ni faraja kubwa sana kwa wadau wa elimu hapa nchini.Hii ni kutokana na ukweli kuwa sera hii ilileta mapinduzi makubwa sana katika sekta ya elimu ambayo hayajawahi kushuhudiwa tangu enzi za azimio la Arusha.Mapinduzi yaliyoletwa na sera hiyo ni kutokana na ukweli kuwa sera hiyo ilitokana na utafiti wa kina uliofanywa ili kutambua hali halisi ya elimu yetu na changamoto zake.Ujio wa sera hii ndio uliopelekea mabadiliko makubwa ya mitaala ya elimu yangu ya awali hadi elimu ya juu.

Miaka michache tu tangu kuingia na kuanza kutumika kwa mitaala hiyo iliyoandaliwa kwa misingi ya sera ya elimu na mafnzo ya 1995,nchi ilishudia mabadiliko mengine makubwa ya mitaala kwa kigezo chenye mashiko cha dhana ya “Ufundishaji unaozingatia ujenzi wa maana”.Haijulikanai ni utafiti kiasi gani ulifanyika ili kubaini udhaifu na ubora wa mitaala iliyokuwepo?! Kama hiyo haitoshi,mara tu baada ya mabadiliko hayo ya mitaala serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi ikatangaza kufanyika kwa mabadiliko ya sera ya elimu-mswada unasubiri Baraka za bunge kuidhinishwa rasmi na kuwaacha wanazuoni midomo wazi na maswali mia kidogo;mathalani Mabadiliko ya sera na mabadiliko ya mitaala kipi kilipaswa kuanza? Je, ni utafiti kiasi gani umefanywa ili kujiridhisha kuwa sera ya elimu na mafunzo iliyopo haijatuletea tija na hivyo haitufai katika dunia ya “ulaji na uteja”[utandawazi na soko huria]? Ikiwa utekelezaji wa mitaala huongozwa na sera na kusimamiwa na sheria zinazoundwa ina maana kuwa mitaala yote iliyoandaliwa kati ya 2006 na 2008 na mingine kuanza kutumika rasmi 2009 itapaswa kubadilishwa ili kuenda sambamba na matakwa ya sera! Je, ni utashi gani tuliotumia kufanya haraka ya kubadili mitaala kabla ya kujua mahitaji halisi ya sekta ya elimu?Je, ikiwa hatukusudii kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu hivi karibuni mswada wa sera ya elimu uliopo mezani una maana gani kwetu?Je, ubadilishaji holela wa mitaala pasipo kufanya upembuzi yakinifu ili kujua hali halisi ni matumizi sahihi ya pesa za wavuja jasho wan chi hii?Hakika maswali ni mengi ila majibu yanaweza kuwa ni mengi zaidi!.

Chimbuko la makala hii ni hofu iliyochipuka kutokana na mambo makubwa mawili;Kwanza ni ripoti ya tathimini kuhusu uwezo wa kujifunza katika elimu hapa nchini iliyotolewa na asasi ya Uwezo Tanzania na pili ni mabadiliko ya fedha yaliyotangazwa hivi karibuni.

Matokeo ya ripoti ya Uwezo Tanzania ni dhahili kuwa imewashitua watu wengi. Lakini kwa wafuatiliaji wa mabo hilo ni jambo lililotarajiwa na hali hiyo kihalisia inaweza kuwa ni mbaya zaidi ya matokeo ya utafiti huo. Aidha hofu yangu kutokana na mabadiliko ya pesa yaliyotangazwa hivi karibuni ni kutokana na ukweli kuwa mabadiliko hayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kupelekea mabadiliko mengine ya mitaala hata kabla ya sera mpya ya elimu kuanza kutumika.Hii ni kutokana na ukweli kuwa fedha yetu ni moja ya alama za taifa letu na watoto wetu kwa kutumia mtaala uliopo wanajifunza juu ya alama hizo.Mfano,katika somo la hisababti darasa la tatu sura ya 3 mwanafunzi anajifunza kuhusu utambuzi wa fedha. Aidha katika darasa hilo hilo la 3 katika somo la Uraia sura ya 3 mada ya 6 anajifunza kuhusu fedha kwa lengo la kumwezesha mwanafunzi kutambua,kutathimini na kuheshimu alama za utambulisho wa taifa lake.Kwa mujibu wa muhtasari uliopo mwanafunzi anatarajiwa kufikia lengo tajwa hapo juu ikiwa ataweza kuainisha na kutaja alama zilizopo katika sarafu na noti za Tanzania.Noti zote zilizoainishwa katika mtaala huo ndizo zinazobadilishwa!!!Hii ina maana kuwa noti mpya na hizi zinazotumika sasa pamoja na kuwa na thamani sawa zitakuwa na alama zinazotofautiana.Kwa kuwa tumejifunza kukurupuka katika kufanya maamuzi,ni dhahili kuwa mihtasari hiyo itarekebishwa haraka ili kukidhi haja. Wakati zoezi hilo likikamika,sera mpya ya elimu itakuwa tayari na ni wazi kuwa maboresho mengine ya mtaala yatafuata!?Je ,katika hali kama hiyo tutarajie kitu gani? Je, ni lini mitaala yetu itatengemaa na hivyo kuwa na tahimini ya mtaala yenye mantiki? Je, ni nini hatma ya elimu yetu katika muktadha huu? Je, walimu,waelimisha walimu, watunga sera na wadau wengine wa elimu tunafanya nini katika hali hii?.