Tuesday, September 30, 2008

CWT kwa maslahi ya nani?Walimu,Serikali au Viongozi?

Mwalimu House ni moja ya majengo mazuri yanayoupamba mji wetu wa Dar si salama.Picha hii inayoonekana hapo ilichukuliwa wakati ujenzi wa jengo ukiendelea.Mwalimu House ni jengo linalomilikiwa na chama cha Walimu Tanzania [CWT]. Ni moja ya miradi mizuri iliyobuniwa na chama katika kuendeleza na kutunisha mfuko wa chama.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na mijadala mikali katika mitandao ya kompyuta kuhusu mapato na matumizi ya fedha za chama.Kwa hakika sijui kusudio hasa la madai hayo ingawa wengi wa wachambuzi wa mambo wanayaelezea kama sehemu ya serikali kupitia kwa watu wake kujibu mapigo kwa viongozi wa chama ambao mara nyingi wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania maslahi ya walimu nchini.Jambo hili linakuwa ni rahisi kuingia akilini mwa watu kutokana na ukweli kuwa madai ya wanachama hao wachache yamekuja siku chache tu baada ya chama kusimama kidete kuishinikiza serikali kulipa madeni yote ya walimu kwa muda muafaka japo bado hilo halijafanikiwa ipasavyo.

Aidha,mjadala mwingine wenye madai mazito kuhusu makato ya ada za uanachama wa CWT ambayo inakatwa kwa asilimia ya mshahara wa kila mwanachama na serikali kutuhumiwa kuhusika katika kushinikiza kila mwalimu awe mwanachama wa CWT na michango yao kukatwa moja kwa moja na Hazina kinyume na taratibu za trade union zingine duniani ni kizungumkuti kingine kwa CWT na serikali kwa ujumla.

Nisingependa kuzungumzia sana kuhusu jengo la mwalimu house wala aina nyingine yoyote ya kitega uchumi cha CWT. Ila nalazimika kuchangia kuhusu makato ya ada ya uanachama na aina za wanachama wa CWT.Kwa maoni yangu nadhani huu ni wakati muafaka kwa serikali na CWT wenyewe kuangalia upya kiwango cha ada ya uanachama ambayo kila mwanachama atapaswa kuchangia tofauti na ilivyo sasa ambapo kiwango cha ada hutofautiana kulingana na kiwango cha mshahara wa mtu.Trade union zote ninazozifahamu zinatoza Ada ya uanachama kiwango kilicho sawa kwa wanachama wake wote.

Aidha kuhusu uanachama wa CWT katiba ya chama ipo wazi .Imejaribu pamoja na mapungufu yaliyopo kufafanua nani ni mwanachama na aina za uanachama.Kutokana na hali hiyo ni vema kwa chama kuitetea na kufuata katiba yake kwa kuwatoza ada ya uanacha wale tu wanaoitwa wanachama hai na sio kumkata kila mwalimu ada ya uanachama kwa kisingizio cha taaluma yake ya Ualimu.Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa wengi wa wanaokatwa ada hiyo ni walimu wale tu walio watumishi wa serikali kwa kuwa ni rahisi sana kujimegea kamkate kao kutoka hazina jambo linalotufanya wengi tujiulize chama hiki ni kwa manufaa ya nani?Je, hizi kelele zinazopigwa na viongozi wake zinamaanisha nini ikiwa chama na serikali lao moja?Kwa hakika mimi sijui.

CWT na serikali kwa ujumla nadhani huu ni wakati muafaka wa kujipeleleza na kuangalia nini cha kufanya kabla jeshi hili kubwa zaidi la watumishi wa umma nchini halijainuka na kuleta dhahama kubwa.Ndio wataamuka tu muda sio mrefu.Wengi wao hasa wa kuanzia miaka ya mwishoni mwa 1990s` hawajawahi kuingia mkataba na CWT kuwa wanachama.Hawana membership number wala kadi.Je,wakidai warejeshewe makato yao tangu walipoanza kazi na kukatwa ada isivyo halali watakuwa wamekosea?Hili ni bomu linalotakiwa kuteguliwa haraka iwezekanavyo. Na kwa nini tusubiri hali hiyo itokee.

Kazi ya mja kunena nami nimenena.