Sunday, March 15, 2015

CWT: JIBU RAHISI KWA MASWALI MAGUMU!





CWT ni trade union iliyo mstari wa mbele kuhakikisha walimu hapa nchini wanapata stahili zao kwa wakati.Pamoja na ukweli kuwa CWT imejitahidi sana katika kutekeleza wajibu huo bado CWT ina mapungufu kadhaa ya kimuundo na kiutendaji. Makala hii inajadili maswala yahusuyo uanachama, makato ya ada ya uanachama na muundo wa benki ya walimu kuelekea katika uchaguzi mkuu wa CWT.

Nimekuwa nikiandika mara nyingi kuhusu uanachama wa mwalimu katika CWT. Katiba ya CWT inasema wazi kuwa kuna aina tatu za wanachama wa chama hicho, mosi ni wanachama wa heshima ambao hupewa uanachama kutokana na mchango wao kwa CWT,Aina ya pili ni uanachama wa hiari na tatu ni wanachama wa halisi ambao wanatoa ada ya uanachama kila mwezi.Upungufu uliopo katika kipengele cha wanachama ni katiba kutotoa maelezo ya kutosha kuonyesha namna ya upatikanaji wa hao wanachama halisi.

Makato ya ada ya uanachama ni upungufu mwingine wa CWT. Tangu nimeifahamu CWT haijawahi kuwa na kiwango sawa cha makato ya ada ya uanachama kwa wanachama wake.CWT imekuwa ikikata 2% ya mshahara wa kila mwalimu kila mwezi kama ada ya uanachama. Kwa maswala hayo mawili ya uanachama na makato ya ada kwa asilimia 2% ya mshahara wa mwalimu kila mwezi ni tatizo linalohitaji ufumbuzi wa haraka. Uvunaji wa pesa za walimu isivyo halali kila mwezi na kutufanya tujiulize hivi CWT ni kwa maslahi ya nani? serikali, AU Viongozi wake?

Nasema CWT inavuna pesa za walimu isivyohalali kila mwezi kutokana na ukweli kuwa kwa sheria zilizopo cwt haina mamlaka ya kuchukua ada ya uanachama kwa % ya mshahara wa mtumishi.Nasema hayo kwa kuwa sheria zote tangu ile ya mwaka 1961,"The organisation of Tanzania Trade Union Act,1961, the trade Union(Revocation of special powers) Act,1962,The Trade Union ordiance Act,1962,"The Trade Unions and Trade Disputes (Miscellaneous Provision)Act, 1964 hadi hii ya sasa iliyofanyiwa marekebisho 2006. Hakuna mamlaka ya aina hiyo isipokuwa kwa sheria ya "Employment and Labour Relations Act,2004(4) inayotoa mwongozo wa nini kifanyike kuhusu makato [Si kwa %] ya mshahara kwenda trade union husika. Kwa mantiki hiyo,CWT imekuwa ikuvuna mabilioni ya pesa isivyo halali kila mwaka kutoka kwa walimu pasipo ridhaa yao.


Aidha,siku za hivi karibuni, kila mahali pa kazi kwa walimu gumzo kubwa ni uchaguzi wa CWT. Walimu wanapigana vikumbo kuhakikisha wanapata nafasi ya uwakilishi au uongozi ndani ya CWT.Huo ni upande mmoja wa shilingi. Upande wa pili wengine wanatafakari nini cha kufanya kutokana na CWT  kuweka masharti yanayowanyima fulsa ya kushiriki katika chaguzi hizo.Moja ya masharti hayo ni mwanachama kuwa ametoa ada ya uanachama kwa kipindi cha miezi kumi na mbili mfulululizo.

Swala la kigezo cha ada napenda nilijadili kwa kirefu kidogo. Hapo juu nimeeleza kuwa kuna walimu ambao kimsingi hawajawaridhia makato ya mshahara wao kwenda CWT lakini wamekuwa wakikatwa. Kuanzia septemba mwaka jana baadhi ya walimu hao wameondolewa makato hayo na baadhi wakiendelea kukatwa makato ya ada ya CWT.Pamoja na Viongozi kutambua CWT imekuwa ikipata mgao toka hazina kama makato ya ada ya uanachama kwa walimu hao ambao kwa sasa hawapo katika makato, waliamua kuweka “kizingiti” kwao ili wasipate fulsa ya kuchagua au kuchaguliwa hata kama walikuwa wakikatwa ada kwa muda mrefu kiasi gani. Hii si sawa hata kidogo!Jambo hili linaleta maswali zaidi ya majibu yanayotolewa kiasi cha kufanya wengine tupoteze imani kwa chama. Viongozi wa CWT wanakiri kuwa kuna walimu wameondolewa makato ya ada ya uanachama na njia pekee ya uchangiaji inayotumiwa ni mwajiri kukata mshahara wa mwalimu na kupeleka katika CWT.Ikiwa makato hayo yamesimamishwa. Je ni nani anayewajibika na kusimamishwa huko ikiwa mwalimu hajawahi kuomba kusimamishiwa makato?.Je, ni halali mwalimu kunyimwa haki ya kushiriki shughuli za chama wakati ameshachangia zaidi ya miaka kumi?Ikiwa alikuwa amekatwa kimakosa,[kama hajawahi kuridhia makato hayo] Je,kwanini chama kisirejeshe  makato hayo kwa mwalimu?.Je,ni hatua gani CWT imechukua baada ya kuona mapato yatokanayo na ada za uanachama yamepungua? Je, CWT haioni kuwa si sahihi kumzuia mwalimu aliyechangia kushiriki katika shughuli za chama?

Uanzishwaji wa benki ya walimu ni wazo zuri ninaloliunga mkono.Viongozi wa CWT  wanapita maeneo ya kazi kuhamasisha walimu kununua hisa ili umiliki wa benki hiyo kwa sehemu kubwa uwe chini ya walimu. Aidha, taarifa zinaeleza kuwa kila mwanachama hai wa CWT atanunuliwa hisa kupitia michango yake ya kila mwezi aliyoyochangia. Hofu yangu bado ipo kwa walimu ambao wameondolewa katika makato hayo.Je, hawa hawana haki ya kushiriki pia katika shughuli za benki ya walimu? Vipi kuhusu hatma na thamani ya michango waliyokwisha changia CWT?. Tunahitaji majibu yenye mashiko kutoka CWT.

Naandika  makala hii kwa CWT na walimu kwa ujumla kwa kuwa naamini kwamba kitendo cha kuwanyima fulsa walimu kushiriki kikamilifu katika shughuli za CWT ni jibu rahisi kwa maswali magumu. Naamini walimu ni waelewa na wenye hekima.Nao watatumia busara zao kulitathimini jambo hili na kulitafutia ufumbuzi. Aidha ,nawaandikia watanzania kwa kuwa naamini kuwa wao ni watu makini na wenye busara ambao hawapo tayari kuona uonevu ukifanywa katika jamii yao.