UTANGULIZI:
Kwa ujumla Sera mpya inashughulikia masuala muhimu na ya msingi kama vile kupunguza umri wa kuanza shule kutoka miaka saba hadi mitano; kuwekwa kwa utaratibu wa kuwatambua na kuwaendeleza watoto wenye vipaji maalum; kuanzisha polytechnics; kuongeza masuala ya TEHAMA na UJASIRIAMALI kwenye mtaala; pamoja na masuala mtambuka.
MAONI:
Kifungu Na 5.3 (elimu ya chekechea) Tamko Na. 4 na 5.4 (elimu ya awali) tamko la 3; na 5.5 (elimu ya msingi) tamko la 7 katika suala la ufanisi katika kutoa elimu bora ya msingi kwa wote na Tamko Na. 1 na 2 kwenye suala la kubaini na kuendeleza vipawa na vipaji vya watoto.
Matamko yote haya yanahusu kuwekwa kwa utaratibu wa kuwatambua watoto wenye vipaji katika vituo vya chekechea, madarasa ya elimu ya awali na shule za msingi kwa lengo la kuwaendeleza katika ngazi za juu. Hata hivyo nia hiyo haijaakisiwa kwenye kifungu 5.7 kichohusu Elimu ya Ualimu. Hapana budi kuwepo tamko la sera linalotilia mkazo kutolewa kwa mafunzo mahsusi kwa walimu (kazini na tarajali) katika ngazi zote kuhusu utambuzi na uhuishaji wa vipaji na vipawa vya wanafunzi. Hali kadhalika, tamko hilo lijumuishe umuhimu wa kuandaliwa kwa walimu ambao pia watakuwa washauri wa mieleko na kazi (Career counsellors). Ni dhahiri kuwa mafunzo ya hivi sasa yanayotolewa vyuoni hayakidhi haja hizi.
Pia hapana budi mfumo rasmi wa upimaji uwe na tamko juu ya kuwekwa kwa utaratibu utakao tilia mkazo na kusaidia uibuaji wa vipaji
Kifungu Na 6. 9 Utawala bora liongezwe tamko la sera lenye kuelekeza kuwa serikali itajuisha misingi ya utawala bora kwenye mtaala wa elimu katika ngazi mbali mbali ili kuwaandaa wananchi wenye fikra huru, wenye kujiamini, wazalendo na wawajibikaji na wenye kuhimiza uwajibikaji wa serikali na viongozi.
suala:
Utoaji wa chakula kwa wanafunzi
Pamoja na sera ya elimu na mafunzo ya 1995 tamko la sera 3.2.7 kuainisha kuwa serikali itaboresha programu za lishe na afya katika shule za msingi na vyuo; upo ushahidi kwamba zoezi hili ambalo umuhimu wake umethibitika na kuthibitishwa kitaalamu kwa tafiti mbalimbali, halikuweza kufanikiwa sana. Tafiti mbali mbali zinaonyesha kuwa, mbali ya maeneo yenye programu za utoaji chakula zinazosaidiwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kama Dodoma, Singida na Manyara na Arusha, pia yale yanayosimamiwa na miradi ya kijamii kama baadhi za wilaya za mkoa wa Kilimanjaro n.k; maeneo mengine ya nchi hayakuweza kufanikiwa sana katika kutekeleza zoezi hili.
Watoto wengi hususan wanatoka familia maskini zaidi wameendelea kwenda shuleni bila chakula. Wengine wamekuwa wakitoroka na wengine kuacha shule kabisa. Badala ya kutamka kimkakati zaidi, sera mpya imelieleza suala hili kijuujuu tu kama suala la huduma muhimu shuleni na vyuoni (Ukurasa wa 68), ambapo tamko la sera linaelekeza jukumu la serikali kuwa ni kuhimiza wazazi, jamii, serikali za mitaa na wadau wengine kuhakikisha kuwa huduma ya chakula bora......
Pendekezo.
Liongezwe tamko la sera kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau itaanzisha mpango kabambe wa utoaji chakula bora kwa wanafunzi wa shule za msingi wawapo shuleni ili kuwavutia kubaki shuleni na kuhakikisha wananufaika ipasavyo na matendo ya kujifunza.
Suala la usawa wa kijinsia:
Tamko Na. 6 kuhusu kuwekwa utaratibu wa kuwawezesha wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua; halina budi kukamilishwa na tamko jingine lenye kuelekeza kuwa serikali itaifanyia mapitio sheria ya elimu na kuelekeza namna ya kuwabana watu wanaowapa mimba watoto wa shule na kudhibiti mazingira yanayopelekea watoto wa shule kupata ujauzito.
suala la makundi yenye mahitaji maalum.
kuwepo na tamko kuwa serikali itaelekeza utaratibu wa kuandaa mazingira rafiki, ikiwemo ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi na walimu wenye ulemavu mbali mbali
Kuhusu suala la ufundishaji wa lugha: ukurasa wa 77
Kufuatia maelezo kuwa Kiswahili ni lugha adhimu ambayo nyumbani kwake ni nchini Tanzania hapana budi kuitazama lugha hii kuwa na hadhi zaidi ya kiingereza. Lugha ya Kiswahili ni tunu ya kipekee kwa nchi zaidi ya au sawa na mlima Kilimanjaro. Kiswahili ni miongoni mwa raslimali ambazo Tanzania inaweza kuzipeleka duniani katika dunia ya kitandawazi kwani imezidi kukua duniani.
Licha ya kigugumizi cha kuamua kuwa na lugha moja ya kufundishia nchini (KISWAHILI) Kuwepo na tamko la sera lenye kuelekeza kuwa wizara yenye dhamana ya elimu kwa kushirikiana na wizara nyingine kama yenye dhamana ya utamaduni na ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa itatoa maelekezo ya kukipa Kiswahili kipaumbele kama raslimali ya kipekee, kuikuza na kuitangaza, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wahitimu mahiri wa lugha hii na kuendesha kampeni kabambe ya kuiingiza kwenye ulimwengu wa TEHAMA.
Suala la mfumo wa michepuo
Ukurasa wa 28 Tamko Na. 1 kuhusu kupanuliwa na kuendelezwa kwa utaratibu wa michepuo ya kilimo, biashara, ufundi na sayansi kimu.
kwa kuzingatia kuingizwa masuala ya TEHAMA na UJASIRIAMALI sambambaa na masuala mtambuka kwenye mitaala/mihtasari, ni vema sera itamke wazi kuwa itaifanyia mapitio mitaala ya masomo ya mchepuo (kilimo, biashara nk) ili kuifupisha na kuifanya iwe ya kivitendo na kijasiriamali zaidi au ikazie maarifa na stadi zinazopatikana kwenye mafunzo ya ujasiriamali. Vinginevyo hakuna faida kuwajazia wanafunzi mambo mengi ambayo hawataweza kumudu kuyashika.
CHANGIA
BALOZI KOMBO AONGOZA MKUTANO WA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA
USALAMA SADC
-
Mkutano wa Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umefanyika Zanzibar tarehe 04 Januari,
2025 chini...
4 hours ago
No comments:
Post a Comment