Wednesday, August 26, 2009

Tunapoandaa walimu wa Sayansi Pasipo "Sayansi"

Wiki iliyopita wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi ilitoa miongozo mipya [Sylabus] kwa ajili ya kufundishia katika vyuo vya Ualimu kwa ngazi zote za cheti na stashahada. Pamoja na ukweli kuwa kwa kiasi fulani upimaji katika somo la Sayansi kwa njia yaVitendo umezingatiwa katika muhtasari hiyo Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni umebainisha kuwa vyuo vya Ualimu 16 vya serikali hapa nchini havina maabara kwa ajili ya mafunzo ya somo la sayansi kwa vitendo.Kutokana na hali hiyo kwa muda mrefu sasa Balaza la Mitihani la Taifa limekuwa likiwatahini walimu katika ngazi ya Diploma na Cheti kwa njia ya Nadharia jambo linalopelekea kufa kwa misingi ya Sayansi kwa wanafunzi na walimu wetu.

Kama wadau wa Elimu hapa nchini tufanye nini kurekebisha hali hii? TAFAKARI!!!!

Thursday, August 20, 2009

BORA CCM WAKISIKZA MANENO YA BABA WA TAIFA

Anaweza kuwa alifanya makosa, alikuwa binadamu;
Wanaweza kutofautiana naye nia kama viongozi, aliipenda zaidi Tanzania;
Wanaweza kujifanya wanamuenzi kinafiki; walianza tangu zamani;
HATA HIVYO NI VEMA, WAKASIKIZA NA KUZINGATIA MANENO YA MWALIMU ILI CHAMA NA TAIFA LISIENDE MRAMA:

"Kila mtanzania, kila mtu kijijini, kila mjumbe wa halmashauri ya wilaya, kila mbunge n.k lazima aweze kusema kwa uhuru bila hofu ya vitisho ama katika mkutano ama nje ya mkutano" J. K. Nyerere (1974) kwenye Binadamu na Maendeleo


"Watu wenye mawazo tofauti, hata kama wakiwa wachache, lazima wawe na haki ya kutoa mawazo yao katika majadiliano bila ya hofu ya kusumbuliwa; mawazo yao na yashindwe katika hoja za majadiliano, siyo kwa vitisho au mabavu." J. K. Nyerere (1974) kwenye Binadamu na Maendeleo.

Nawasilisha

Saturday, August 15, 2009

Serikali: Bingwa wa sanaa za Maonyesho kuhusu machapisho ya Kielimu.


Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia mijadala kabambe inayohusu sekta ya elimu hapa nchini.Maslahi na Uwajibikaji wa walimu,Lugha ya Kufundishia na Kujifunzia na Machapisho ya Lielimu ni Baadhi tu ya maswala yaliyoshika kasi katika mijadala ha hivi karibuni.

Kwa mtazamo wangu "Finyu", matatizo katika elimu yetu ni ya ki-mfumo zaidi.Na msururu wa matatizo katika elimu ni zaidi ya hayo yaliyoainishwa hapo juu.

;eo ningependa kuendelea kuchangia mjadala kuhusu machapisho ya kielimu kama nilivyopata kuandika siku za nyuma.Nimeshawishika kuandika ili kuchangia mjadala huu kwa kuwa mwelekeo wa mjadala huu haupendezi machoni pangu.Hapo awali nilizoea kusikia kutoka kwa wanasiasa lawama zao juu ya Vitabu vya kiada katika shule zetu na machapisho mengine ya kieleimu, malalamiko hayo siku zote niliyapuuza kwa kuwa niliamini hawajui wanacholaumu!!!.Nimeingiwa na woga baada ya kuona hata Watu wenye "Visomo Vilivyotukuka" na wenye kuheshimika katika jamii yetu wakujadili jambo hili kama "Walevi" [Sijui ndio wameleweshwa kwa uchawi wa Gining?].Hakika tunahitaji kuwa na mjadala makini kwa kuweka kando "Ushabiki" kwa maslahi ya taifa letu.

Katika kujadili swala la vitabu vya kiada na machapisho ya kieleimu kwa ujumla, ni vema tukarudi nyuma kidogo miaka michache iliyopita kabla ya kutungwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 ambayo ndiyo iliyopelekea mabadiliko yote tunayoshuhudia leo hii katika elimu yetu. Ni wazi kuwa katika kipindi hicho elimu yetu ilikuwa taabani katika kila wigo: Ubora, Upatikanaji, Utolewaji wake na miundo mbinu-japo kwa uchache. Kutokana na hali hiyo,sera ya Elimu na Mafunzo-1995 ilikuja na mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta Elimu.

Pamoja na mambo mengine, katika utekelezaji wa mpango wa Uboreshaji wa sekta ya elimu,Serikali kupitia wizara ya elimu ilianzisha kamati maalumu ya kutathimini machapisho ya kielimu-EMAC ili kudhibiti ubora wa machapisho ya kielimu baada ya sekta binafsi kupewa fulsa ya kuchapisha vitabu ili kukidhi upungufu mkubwa wa vitabu uliokuwepo katika shule zetu.[Rejea waraka wa Elimu No. 2,1998]

Aidha, kwa mujibu wa waraka wa Elimu No. 7 wa Dec. 2005 ambao ulichukua nafasi ya waraka wa elimu namba 2 wa mwaka 1998 ambao ulianzisha EMAC, machapisho yote ya kielimu yanayopaswa kutumika kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya Ualimu Tanzania Bara hayana budi kupata ITHIBATI ya wizara ya elimu kupitia EMAC.

Shughuli ya kutathimini machapisho ya kielimu ilianza rasmi mwezi Novemba 1999 na vyeti vya ithibati vilianza kutolewa rasmi kwa machapisho yaliyoidhinishwa kuanzia januari 2000.Tangu hapo wizara imekuwa ikitoa orodha ya machapisho yote yaliyopata ithibati kila robo mwaka na kuisambaza kwa wadau wa elimu katika ngazi zote ikiwa ni pamoja na asasi na taasisi zisizo za kiserikali.

Katika kuhakikisha kuwa kila chapicho la kieleimu linakuwa na ubora unaotakiwa, serikali kupitia wizara ya elimu desemba 2005 ilitoa mwongozo wa namna machapisho yote ya kielimu yatakavyokuwa yakitathiminiwa.Pamoja na mambo mengine,mwongozo huo unaonyesha wajumbe wa EMAC, Vigezo vya kutathimini, mchakato wa kutathimini,utolewaji wa cheti cha ithibati na Rufaa.Kwa mujibu wa mwongozo huo EMAC inaundwa na wajumbe 15 kutoka sekta binafsi na serikalini na inajumuisha hawa wafuatao:
1. Afisa Elimu Kiongozi wa Wizara [M/kiti]
2. Mkaguzi mkuu wa shule
3. Mkurugenzi Elimu ya Ualimu.
4. Mkurugenzi Elimu ya Sekondari.
5. Mkurugenzi Elimu ya Msingi.
6. Mkurugenzi Taasisi ta Elimu Tanzania.
7. Mkurugenzi, sera na mipango-wizara ya elimu.
8. Mshauri wa kisheria wa wizara.
9. Mwakilishi-Shilikisho la wauza vitabu [BSAT]
10. Mwakilishi wa shilikisho la wachapishai vitabu-[PATA]
11. Ofisa mwandamizi,chama cha haki miliki Tanzania [COSOTA]
12. Mwakilishi wa wachapaji[Printers]
13. Katibu mtendaji,Umoja wa wamiliki wa shule na vyuo binafsi.
14.Mwakilishi-Mkuu wa kitivo,kitivo cha Elimu kutoka katika moja ya vyuo vikuu hapa nchini
15.Mjumbe mmoja wa kuteuliwa na Katibu mkuu-WEU Kutoka miongoni mwa watu katika sekta binafsi mwenye uelewa wa kutosha na uzoefu katika soko la Vitabu.

Nimejaribu kuainisha muundo wa kamati ya kutathimini machapisho ya kieleimu-EMAC ili kutoa picha ya aina ya watu waliopewa dhamana katika kuhakikisha ubora wa machapisho yote yanayopekekwa mashuleni.Jambo la kusikitisha baadhi ya watu walioshiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa mabadiliko katika sekta ya elimu na kutufikisha hapa tulipo leo hii wanakuja na " Mashairi" ya kutaka kurudi tulikotoka!!!Wanalalamika kuwa kuna machapisho mengi hayakidhi haja na wingi wa machapisho hayo unawakanganya walimu!!!!Kwangu hoja zinazotolewa hazina mashiko hata kidogo. Machapisho yasiyokidhi haja kama yapo ni Upungu/udhaifu wa nani? watendaji au mfumo? Kama ni mfumo,Je ni utafiti wa kina kiasi gani tumeufanya ili kuthibitisha madai hayo? Je, upembuzi yakinifu umefanya kuweza kubaini madhara yanayoweza kutokana na haja tunayoililia? Kwangu, "Kilio cha kurudi katika ukiritimba wa utumiaji wa kitabu kimoja" ni aina nyingine ya maigizo yanayoashiria upungufu katika uwajibikaji wa watu waliopewa dhamana ya kustawisha jamii yetu!!!

Ikimbukwe kuwa kabla ya waraka wa elimu namba 2 wa 1998, shughuli zote za uandaaji wa mitaala na uchapaji wa machapisho ya kielimu ilikuwa chini ya Taasisi ya Elimu Tanzania.Kwa mujibu wa waraka huo,shughuli zote za uchapishaji ziliachwa katika soko huria na serikali kupitia Taasisi ya Elimu imebaki na jukumu la Kuandaa miongozo[ Sylabus] ambayo kwayo waandhishi na wachapishaji wanapaswa kuizingatia katika uandaaji wa machapisho yao.Pamoja na mambo mengine hebu tujiulize, kabla ya kuingia katika mfumo tulionao tafiti mbalimbali nyingi zilifanywa na kubaini mapungufu yaliyokuwepo katika elimu yetu:
1. Je , matatizo yaliyoainishwa na tafiti zilizopelekea tukawa na machapisho mengi yametatuliwa
kwa kiasi gani?
2. Je, serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa mapungufu hayo hayatokei tena?
3 Mwisho wakati wa utekelezaji wa waraka wa elimu namba 2 wa mwaka 1998, serikali kupitia TIE
mwaka 2004 iliingia mkataba na makampuni binafsi na kuiuzia shehena yake yote ya Vitabu
ilivyokuwa imeandaa ili kuepuka hasara.Je, sekta binafsi itafidiwa vipi kwani imewekeza sehemu
kubwa ya mtaji wake katika uchapishaji wa vitabu?

Mwisho napenda kuwakumbusha wale wanaolia kuwa wingi wa vitabu maashuleni "unawakanganya walimu" kuwa kilio chao hakina mantiki kwa kuwa vitabu vyote vilivyopo shuleni tunategemea kuwa vimeandaliwa kwa kuzingatia miongozo iliyopo na vimekidhi mahitaji na ndio maana EMAC wameidhinisha vitumike kufundishia.Aidha ikumbukwe kuwa walimu wote, moja ya mabo wanayojifunza wakati wanapokuwa chuoni[ Katika kozi ya Ualimi] ni namna ya kutathimini Ubora wa vifaa vya mtaala.Hivyo hija ya kuwachanganya hapo haina mashhiko kabisa!!!!. Kulilia ufundishaji kwa kutumia kitabu kimoja ni kuwanyima walimu fulsa ya kupenda kusoma na kutathimini ubora wa aina ya kifaa cha kufundishia.

Inawezekana kabisa kuwa wanaolalama kuwa vitabu vingi vinawachanganya walimu hawana A,B,C za ualimu. Na kama wanazo basi kwa maslahi yao binafsi wanaamua kujifanya hawajui.Ajabu Wizara ya Elimu Imekaa na Taasisi ya Elimu imekaa kimya pasipo kutoa tamko lolote kuhusu udhibiti uliopo wa ubora wa machapisho ya kielimu. Sijui wanafanya hivyo kwa maslahi ya nani?

Sishangai sana kusikia walimu wanachanganyikiwa na wingi wa vitabu vya kufundishia.Nimekuwa katika taaluma ya Ualimu kwa muda sasa.Uzoefu nilioupata unaonyesha kuwa walimu wengi ni wavivu wa kujisomea.Hao ndio wanaolalama!!!?Wamezoea kulishwa.Na ndio maana sio ajabu ukipita mashuleni ukaona mwalimu anatumia maandiko [notes] alizosomea yeye miaka ya 80 au 90 akiamini kuwa ni bora na kusahau kuwa mitaala imebadilika.

Hivi ni kwanini bila kujali nguvu, muda na rasilimali tulizowekeza katika mabadiliko tuliyofanya juzi tu hata bila kufanya utafiti wa kina leo hii tunalazimishwa /shurutishwa kukubali kuwa tulikosea?!!!!Je, mara hii tumesahau kabisa juhudi zilizofanywa na wadau hasa unesco katika kutafiti na kufanya upembuzi yakinifu katika kubaini matatizo yaliyokuwepo katika elimu?Anyway MUNGU IBARIKI TANZANIA!!!