Friday, July 4, 2008

“Ukinyonga” wa Serikali kuhusu Machapisho ya Kufundishia na kujifunzia.

Leo nimeona niandike kuhusu machapisho yanayotumika katika kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi,sekondari na vyuo vya ualimu hapa nchini.Msingi na chimbuko la makala haya ni “Ukinyonga” wa serikali kuhusu uchapishaji wa machapisho hayo..

Mwanzoni mwa miaka ya tisini tulishuhudia kuzikwa kwa azimio la Arusha na Kuzaliwa kwa Azimio la Zanzibari ambalo liliimarisha[sio kuanzisha] na kuendeleza “wimbo” mashuhuri wa Uhuru wa biashara---soko huria---.Hivyo kumaliza ukiritimba wa baadhi ya taasisi hasa za serikali katika soko jambo lililotuingiza katika zama hizi za “ulaji na uteja”.Hii inatokana na ukweli kuwa serikali kwa dhati iliamua sio tu kutekeleza kwa vitendo sera ya soko “holela” bali pia kujiondoa katika ushindani wa soko [kwa kubinafsisha mashirika ya umma] na kuiachia sekta binafsi.

Kuanzia mwaka 1995 hadi 2000+ tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya Elimu yaliyotokana na sera ya elimu na mafunzo ya 1995.Matokeo ya sera hiyo yalipelekea kuundwa kwa kamati maalumu ya kutathmini machapisho ya kielimu[EMAC] chini ya Wizara ya elimu katika idara ya Sera na Mipango(Rejea waraka wa elimu Na.2 wa 1998)

Kwa mujibu wa waraka huo machapisho yote yanayotumika kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi,sekondari na vyuo vya ualimu Tanzania bara hayana budi yaidhinishwe na wizara ya Elimu kupitia EMAC [Ingawa yale yote yaliyoandaliwa na TET hayana ithibati].Baada ya upembuzi yakinifu na utafiti wa kina kufanyika,serikali kupitia waraka wa Elimu namba 7 wa 2005 iliamua kuipa nguvu zaidi EMAC ili kudhibiti ubora wa machapisho ya kielimu hapa nchini.

Yabidi tufahamu kinaga ubaga ninamaanisha nini hasa ninapozungumzia ukinyonga wa serikali kuhusu machapisho ya kielimu.Kabla ya mabadiliko ya “hali ya Hewa” katika sekta ya elimu nchini,machapisho yote ya kielimu yalitolewa na kusambazwa na Taasisi ya elimu ya Taifa [TET] ambayo imepewa mamlaka kisheria ya kuandaa,kukuza,kusambaza,kusimamia na kutathmini mitaala ya shule za msingi,sekondari na vyuo vya Ualimu hapa nchini. [Rejea Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 sura ya 6 uk.51 Ibara ya 6.2.1]

TET ni taasisi ya serikali iliyochini ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi (MoEVT). Taasisi hii iliundwa kwa sheria Na. 13 ya 1963 wakati huo ikijulikana kama Taasisi ya Elimu(Institute of Education) chini ya chuo kikuu kishiriki cha Dar es salaam.Pamoja na mabadiliko mbalimbali kufanyika,mfano ya kuwa chini ya chuo kikuu cha Dar es salaam na kubadili jina kutoka iliyokuwa taasisi ya elimu na kwenda Taasisi ya ukuzaji mitaala [Institute of Curriculum Development] na sasa Taasisi ya Elimu ya Taifa [Tanzania Institute of Education] malengo ya uanzishwaji wa taasisi hii,kazi ,dhima na dira yake hazijabadilika.

Serikali katika moja ya harakati zake za kujiondoa katika ushindani wa soko kupitia wizara ya Elimu na utamaduni (Sasa Elimu na mafunzo ya ufundi) chini ya Mpango kabambe wa maendeleo ya sekta ya Elimu,mwaka 2004 iliamua kuingia makubaliano na sekta binafsi ili kuziachia kazi za kuchapisha kuuza na kusambaza machapisho yake yote ya kielimu yaliyokuwa yakitumika katika shule na vyuo vya ualimu nchini.Aidha,katika kutimiza azma hiyo serikali ilitangaza zabuni na kuingia mikataba na makampuni binafsi ya uchapishaji kwa lengo la kuyauzia hifadhi yake ya vitabu vya kiada.

Pamoja na ukweli kuwa serikali ilijitoa katika uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya kiada,ziada na rejea,wapo watu wanaoendelea kuulilia “Ukale” na kuitaka serikali irudi katika biashara [Kwa faida ya nani?!].Katika kutaka kutimiza ndoto zao hizo wanatumia nguvu nyingi na fedha za walala hoi kufanikisha azma hiyo.

Kwa harara ya Faru kama sio Mbogo,serikali imeyapokea mapendekezo yao na katika kujaribu ku-justify papara iliyonayo Taasisi ya Elimu ya Taifa [TIE] kupitia kwa kampuni ya ENV consult (T) ltd katika barua yake ya June 20,2008 yenye kumb.Na.TIE/CR/644/08/I/12 imesambaza waswali hojaji [Dodoso] kwa wazazi,wanafunzi,walimu na asasi mbalimbali kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali zitakazosaidia kile wanachodai kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo [Katika uandaaji wa vitabu?!!] ili kukidhi kusudio la uanzishwaji wake.

Nashawishika kusema kuwa utafiti huo ni sehemu ya namna ya ku-justify papara ya serikali kutokana na hofu yangu kuhusu uthabiti wake.Hii inatokana na ukweli kuwa madodoso hayo ambayo kwa sehemu kubwa [Taz swali la 8-13 ]yanalenga kubaini ubora wa vitabu yanapita katika mikono ya watu wengi (Wazazi,wanafunzi na hata baadhi ya walimu) ambao misingi na vigezo vya uchambuzi wa vifaa vya mtaala hawavijui.

Katika kuutafakari ukinyonga wa serikali kuhusu shughuli ya uchapishaji na usambazaji wa machapisho ya kielimu ni vema tukakumbuka kuwa Uamuzi wa kujiondoa ulitokana na pamoja na mambo mengine matakwa ya sera ambayo iliandaliwa baada ya tafiti mbalimbali na za kina kufanyika.

Ninapata Mkanganyiko pale ninapojaribu kutafakari kazi na wajibu hasa wa Taasisi ya Elimu na Uanzishwaji wa EMAC.Aidha,sioni mantiki ya chombo hicho “kuegeshwa” katika idara ya Sera mipango wizara ya elimu badala ya kuwa kitengo katika Taasisi yenye mamlaka na mitaal.In maanisha nini kuueleza umma kuwa TIE pamoja na mambo mengine ina wajibu wa kusimamia na kutathmini mitaala wakati kazi ya kutathmini na kuidhinisha machapisho ya kielimu inaachiwa chombo kingine?! Au ni aina nyingine ya Ufisadi?Kwa nini TIE ing`ang`anie kutunga vitabu na kuacha jukumu lake la msingi kabisa?

Siku za hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kuwa machapisho mengi yaliyoko sokoni hayana ubora unaotakiwa!Jambo la kusikitisha ni kuwa malalamiko hayo yanatolewa na watu waliopewa dhamana ya kuangalia ubora huo.Kihalisia wanaithibitishia jamii kuwa wameshindwa kuwajibika.Hivi inakuwaje bidhaa mbovu zikaidhinishwa na kupewa ithibati wakati chombo cha kusimamia kipo na miongozo ua uthamini ipo na watu wanalipwa mishahara?achilia mbali posho ya kazi hizo?
Hainiingi akilini!!! Ahhh!!!!!!!!


Mungu ibariki Tanzania.

No comments: