Tuesday, September 18, 2007

Pro.Chachage:Msomi wa Jamii ataekumbukwa Daima


Ni mwaka wa tatu  sasa tangu mpendwa wetu Prof. Seithy Chachage alipoiaga dunia. Leo ni siku ya kihistoria kwetu. Ni siku ya kihistoria kwa kuwa tunaadhimisha kumbukumbu ya kifo cha mpendwa wetu, mzazi wetu, mlezi wetu na rafiki yetu. Siku ya leo ni siku inayotuongoza kuyatafakari mambo machache katika maisha yetu yanayoguswa na maisha ya Profesa Chachage (Mungu amlaze mahali pema). Ni siku ya kugeuka na kutazama haiba ya jamii yetu tukizingatia yanayojitokeza katika utashi wa waliotutangulia. Kumbukumbu hii inafanya historia kwetu isiwe mambo ya kale ila mambo yanayotuhusu sasa na kwa matarajio mema ya siku zijazo.

Kwa hiyo basi, historia kwetu iwe ni sasa ikivuviwa na zamani; iwe ni matendo ya sasa yakitiwa nguvu na yale ya waliotutangulia Tunapofanya tafakuri ya maisha ya marehemu Profesa Chachage, ni vema tukaungana na wanafalsafa waliojaribu kuiona historia kama tendo la mtu anayekimbia, akienda mbele anakotaka bila kupafahamu, ila akitazama nyuma kwa tahadhari ya yaliyoishakumgusa.

Kumbukumbu ya leo inatusukuma kuifikia hali ya ukingoni ambayo wanatheolojia wanaiita “ apocalyptic moment”. Hali inayodai ufunuo mpya. Hali tata inayodhihirisha fumbo la maisha yetu . Fumbo hili ni kwamba, kuna pengo kubwa kati ya ukweli wa maisha yetu na jitihada za mantiki tunayotumia ili kuona ukweli huo . Ndio maana tunasimama na kutafakari ;tunatazama maisha ya waliotutangulia ili kupata nguvu za utashi wa sasa unaokidhi haja za kisasa. Tunatafakari maisha ya Profesa Chachage ili tuweze kuyaona maisha yetu vizuri zaidi .Ni kipindi cha kutafakari!

Ujasiri wetu wa kutafakari maisha ya Profesa Chachage huenda ukafananishwa na ule wa Susi na Chuma waliotafakari maisha ya Dr. David Livingstone na kuubeba mwili wake toka Ujiji – Kigoma hadi Bagamoyo akazikwe makwao. Sisi tunatafakari maisha ya mtu aliyeishi pamoja nasi , aliyefanya kazi pamoja nasi. Tunamkumbuka Profesa Chachage kwa mshikamano aliokuwa nao kwetu hadi kufikia mauti yake.

Pamoja na ukweli kuwa ni mwaka mmoja tu tangu alipotutoka,mengi yanayotuzunguka huibua kumbukumbu kumhusu Profesa Chachage. Wengine tumeishi naye ; wengine tumefanya kazi pamoja nae na wengine tumemsikia tu na kuona kazi zake. Hayo yote hudhihirisha azma aliyokuwa nayo katika maisha yake aliyoishi kama “Msomi wa Jamii (Public Intellectual)”

Ninaporejea hotuba kali yenye simanzi ya William Shakespare katika tamthilia ya Julius Kaisari inaonyesha ujasiri wa Marko Antoni katika kumzika Kaisari “…….. maovu watendayo watu hudumishwa baada ya uhai wao , ila mema huzikwa pamoja na mifupa yao…………” Na iwe hivyo kwa Kaisari!”Marko Antoni alisema hayo kwa kuwashutumu mahasimu na Waroma kwa kusahau mema mengi ambayo Kaisari aliwatendea. Nasi leo tunajaribu kuyataja walau machache katika mema mengi ya Profesa Chachage.

Kwa hakika yapo mambo mengi sana mema aliyoyafanya Profesa Chachage katika siku za uhai wake. Profesa Chachage katika uhai wake alijitahidi sana kuitazama haiba ya jamii yetu kwa kuzingatia mambo yanayojitokeza katika utashi wa matendo yetu ili kuleta ufunuo mpya na matarajio mema ya jamii yetu kwa siku za usoni.

Profesa Chachage aliitambua fika “ajali” yetu; ambayo ni kuishi katika bara lililojaa mazonge na madhila, na mzigo wa umaskini. Siku zote alikuwa ni mfuasi mzuri wa dini ya “Ubinadamu” akijitahidi kuikarabati jamii na kupanda mbegu ya ujasiri ili tuweze kuikana mifumo dhalimu inayowalaza watu njaa. Aliamini kuwa tunahitaji uhuru wa fikra na juhudi zetu wenyewe katika kujiletea maendeleo .

Siku zote alikinzana na wasomi wetu ambao wengi wao wamenaswa katika mikoba ya uchawi wa Giningi na kusahau kabisa uganga (Udaktari) ambao wameusomea na kufuzu kwa viwango vilivyotukuka. Alipinga wazi wazi matendo yaliyopanua mpasuko katika jamii baina ya watawala wakwasi wa kupindukia na wananchi maskini hohehahe waishio katikati ya utajiri wa asili.

Kutokana na hulka aliyokuwa nayo ,sio tu aliwaogofya watawala “waliokeneguka” bali pia asasi za kimataifa kila alipokuwa akitoa mwito wa kujali masuala yahusuyo ujenzi wa jamii bora yenye kuzingatia haki , usawa wa binadamu, uhuru , ubinadamu na ukomavu wa kiuchumi. Pamoja na ukweli kuwa juhudi za kujikomboa katika nyanja zote za kujenga Dunia mpya iliyo bora. Mapambano ya kuleta Dunia mbadala ambayo haina ubaguzi, ukandamizwaji, unyonyaji wala ufisadi ina historia ndefu , tangu enzi za mababu zetu. Inasikitisha kuona kuwa kila kukicha wajanja wanakuja na mifumo mipya ya maisha inayotutaka turudi nyuma katika mapambano haya ya kihistoria.

Profesa Chachage hakuna alichopoteza duniani. Alifanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya nchi yetu na kuweka “muhuri” wake katika mioyo ya Watanzania. Kama ilivyo kwa shujaa wa “Mapinduzi” Che Guevara , Profesa Chachage tutaendelea kumkumbuka kwa ushujaa wake. Ushujaa wa kuchukua uamuzi mzito kwa ajili ya watu na si wakubwa fulani. Maombolezo ya kifo chake na umati wa watu waliohudhuria mazishi yake ni ushuhuda wa haya yanayosemwa juu ya Profesa Chachage.

Kwa haraka haraka, anayesikiliza tafakuri hii ya maisha ya Profesa Chachage anaweza kusema kuwa inamhusu mtu mmoja mdogo na mahala fulani padogo (Mtwango au Changanyikeni)! Ikumbukwe kuwa wengi tumepita mikononi mwake na kusambaa katika jamii pana. Kwa njia hii maisha ya mtu mmoja yanaweza kuwagusa wengi hata wale ambao hawakukutana nae. Kutafakari kwetu kutukumbushe mbegu ya haradali.
Ni mbegu ndogo sana, ila hupandwa na kuchipua . Inastawi na kuwa mti mkubwa ambao ndege hutua na kuimba juu yake. Mbegu moja huzaa maelfu na kutokana nayo hupatikana msitu mzito.

Kwa hakika leo hatuombolezi. Hatuna majonzi katika kumkumbuka Profesa Chachage . Jambo lililo muhimu kwetu sasa ni kwamba, katika kumkumbuka tunaweza kuchipuka upya kama mbegu ya haradali. Tujifunze kuwa tayari kusimama , kuhoji na kukataa mambo yote yanayotulazimisha kuyakubali yale tusiyoyaafiki .Mambo yanayopingana na itikeli za maisha yetu. Kumbukumbu ya Profesa Chachage inatukumbusha kuepuka kujiuliza, “Nitapata nini nikitenda mema? Hiki ni kipindi kinachohitaji ufunuo mpya!

“Mungu amlaze mahali pema peponi Profesa Chachage”

Adios Amigo

Profesa Seithy Loth Chachage “Mwamwani”

1 comment:

Anonymous said...

Naomba kupata historia ya maisha ya Profesa Seithy Chachage, alikozaliwa, alikosoma na familia yake!