Nini kikubwa mno unachoweza kututendea leo ambacho
bado hatujajitenda wenyewe?
Utatuambia nini leo ambacho bado
hatujajidanganya nacho?
Huwezi kujua ni miaka mingapi
tumezililia hadi tukaziangulia kicheko
njozi zetu zilizosambaratika na kubaki
vipande vipande.
Ndiyo
Tumeazimia kuyalazimisha matumaini
yetu yaliyokwisha potea kuwa njozi
thabiti kuliko unavyoweza kufikiri:
itangaze ukombozo wetu uliopatikana kwa
uchungu:
Kwa hiyo wala usituulize tunajishughulisha
na nini safari hii:
Mwenye ndoto haisahau hata
ijapokatishwa.
Nawe hutasalimika na hicho
tutakachokifanya.
Kutokana na vipande vya maisha yetu.
Nimeanza mada hii kwa utenzi huo wa mwanazuoni,malenga na mwanaharakati Prof.Abena Busia kwa makusudi ili kujikumbusha na kuikumbusha jamii kuhusu harakati za walimu kutafuta na kudai haki wanazostahili kutoka kwa waajiri wao(Katibu mkuu wizara ya Elimu na Wakurugenzi wa wilaya)
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu sana harakati zinazofanywa na CWT kwa muda mrefu.Hii ni kutokana na ukweli kuwa siku zote huwa najitahidi sana kujustfy wazo langu nililowahi kulitoa hapo awali kuwa CWT sio chama cha kitaaluma(Rejea makala yangu kuhusu CWT na mustakabali wa Elimu nchini)
Ninaporejelea harakati za CWT hasa za viongozi wa ngazi za juu katika chama hicho,nafarijika kutambua kuwa walimu sasa wameutambua unyonge wao na sasa wanaazimia kuukana kama katiba ya chama hicho inavyoleleza katika sehemu ya utangulizi:
“KWA KUWA mwalimu ni kama raia mwingine yeyote nchini
ana haki ya kupata huduma bora za kijamii,kiuchumi
na kimaslahi kama vile afya,chakula,malazi,usafiri na
Huduma nyingine za kijamii.
Kwa hiyo BASI:Sisi walimu wote kwa pamoja tunaazimia
kuungana na kuunda chama chetu kitakachohakikisha kuwa
walimu wote tunatekeleza wajibu wetu na kupata
haki zote tunazostahili kutoka kwa waajiri wetu”
Nimeshawishika kuandika makala hii kutokana na matokeo ya kikao cha pamoja kati ya mawaziri wa TAMISEMI,Elimu,Menejimenti ya Utumishi wa umma na viongozi wa chama cha walimu kilichofanyika Febr. 22 mwaka huu chini ya waziri mkuu ambapo ilikubalika kuwa serikali itawalipa walimu madeni yao yote ifikapo mwezi huu.
Walimu,kwa hakika tuna kila sababu ya kuishinikiza serikali kupandisha mishahara yetu na kutulipa madai yetu mengine kama vile posho za kujikimu,malimbikizo ya mishahara na likizo.Hatuna sababu ya kuchuuzwa na matamshi yasiyomaanisha utatuzi wa matatizo yanayotusonga katika utekelezaji wa wajibu wetu-ndio maana Prof.Abena anatukumbusha kuwa”Utatuambia nini leo ambalo bado hatujajidanganya nacho? Je, ni miaka mingapi tumezililia shatili zetu hadi tukaziangulia kicheko?Ni matumaini yangu kuwa CWT na walimu wote kwa ujumla tumeazimia kwa dhati kuyalazimisha matumaini yetu yaliyokwisha potea kuwa njozi thabiti kuliko mtu yeyote anavyoweza kufikiri.Serikali inapaswa kutambua kuwa mwenye ndoto haisahau hata ijapokatishwa,nayo haitasalimika na kile tutachokifanya.
CWT na walimu kwa ujumla tunachangamoto kubwa katika kuhakikisha tunapata stahili zetu kutoka kwa waajiri wetu.Changamoto ya kwanza ni katika hulka ya itikadi na ya pili iko katika mikanganyiko yetu ya kiuharakati katika jumuia yetu bila kutambua kwa kina kile kinachocho tuunganisha na mipaka yake.
Kujielewa kwa namna ya kutuwezesha kubainisha na kutetete msimamo wetu ni changamoto nyingine tuliyonayo.Tunao wajibu wa kuwa wanafunzi wakati wote tukichambua bila kukoma hali ya walimu na jamii yetu katika enzi hizi za utandawazi ili kujifahamisha njia zinazotumika katika kutunyima stahili zetu na jinsi zinavyobadilika badilika.
Labda kwa kumalizi tu,niwakumbushe walimu kuwa silaha ya mwisho ya kila mfanyakazi Duniani ni kugoma pale anapoona hapati haki zake.Hatua hii ya wafanyakazi hufikiwa baada ya mwajiri kukaidi kusikiliza kilio chao kwa muda mrefu.
Alamsiki!
No comments:
Post a Comment