IMEELEZWA kuwa zaidi ya watu milioni 5, sawa na asilimia 13 ya Watanzania takriban milioni 36, hawajui kusoma na kuandika.
Hayo yalisemwa hivi karibuni mjini hapa na Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Watu Wazima na Mratibu wa Elimu kwa wote kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Salum Manjagila, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa uhamasishaji wa progaramu ya Ndiyo Ninaweza, katika Manispaa ya Dodoma.
Alisema kuwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika nchini imekuwa ikiongezeka kwa asilimia mbili kila mwaka, hali itakayosababisha idadi ya wasiojua kusoma na kuandika kukua iwapo hatua za kukabili hali hiyo hazitachukuliwa.
Alisema hiyo inaonyesha kuwa watu hawajahamasishwa kiasi cha kutosha kuhusu kujifunza kusoma na kuandika, kama njia ya msingi ya kufuta ujinga.
Manjagila alisema mpango huo unafanyiwa majaribio katika mikoa minne ya Mwanza, Ruvuma, Dar es Salaam na Dodoma.
Alisema lengo la mpango huo ni kuhakikisha kuwa watu wasiojua kusoma na kuandika nchini wanatambuliwa na kupatiwa fursa hiyo, na pia kuangalia maeneo ya kuboresha na kuongeza ubora wa elimu ya watu wazima.
Manjagila alisema mpango huo unagharamiwa na serikali, ambako jumla ya sh milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya mafunzo na kiasi cha sh milioni 30 zimetengwa kwa ajili ya kukarabati baadhi ya vituo vya elimu ya watu wazima.
Alisema kuna watu wazima wasiojua kusoma na kuandika lakini wanafahamu mambo mengine makubwa, hivyo iwapo watafundishwa kusoma na kuandika, wanaweza kutumia utaalamu walio nao kuboresha maisha yao.
Naye Ofisa Elimu Kiongozi, kitengo cha Elimu ya Watu Wazima kutoka Wizara vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Regina Nicholaus, alisema utekelezaji wa mpango huo utaanza Oktoba, mwaka huu, watakapokuwa wamemaliza kuandaa kitabu cha mwalimu na mwanafunzi.
Ofisa Elimu ya Watu Wazima wa Manispaa ya Dodoma, Gosbert Damazo, alisema kuwa katika Manispaa ya Dodoma, watu wanaojua kusoma na kuandika ni 137,845, sawa na asilimia 74.2 ya wakazi wote wa manispaa hii na wasiojua kusoma na kuandika ni 47,984 sawa na asilimia 25.8.
Wakichangia katika mkutano huo, wadau wa elimu walisema kuwa waratibu wa elimu wawezeshwe kupata takwimu sahihi na maana nzima ya elimu ya watu wazima.
Author:Fatma Gaffus, Dodoma
Tanzania Daima.
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA CMA KWA UANZISHWAJI WA MFUMO WA KIDIJITALI.
-
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa uanzishwaji wa Mfumo wa Uendeshaji na
Us...
9 hours ago