Tuesday, December 4, 2007

Falsafa ya Elimu-Tanzania

Salaam.

Ni muda mrefu sasa tangu nilipokuandikia.Kaisari amenishika ndugu yangu nikileta ubishi watoto watalala njaa.Leo nimeona nitumie tena muda huu mdogo wa lunch nikuandikie japo kwa uchache ili tuweze kujadili kwa pamoja kuhusu falsafa yetu ya elimu.


Mwalimu! Fumbua macho.Amka mwalimu!!!Ndio,tunapaswa sasa kufumbua macho na kuona mapungufu yaliyopo katika katika jamii yetu.Tusiwe watu wenye dhamira nyepesi na kuyafumbia macho mapungufu hayo kwa kujifariji kwa dhana dhahania zinazotokana na utekelwazaji wa “Elimu ya kujitegemea”kama falsafa ya elimu ya taifa letu.


Neno Falsafa ndugu zangu lina maana ya Taaluma inayojishughulisha na kutafuta ukweli wa jambo kwa njia ya kutafakari.Lakini Falsafa ya Elimu ni utumizi wa falsafa na mbinu zake katika kufafanua maswala ya Elimu mfano maana ya elimu katika jamii na namna ya kujifunza.Hoja hii ya falsafa ya Elimu ya taifa inakuja katika wakati ambao kwetu wengi hatukukitarajia.Kipindi kigumu na chenye mabadiliko makubwa ya ya kiuchumi,kisiasa na kiutamaduni duniani kote jambo ambalo limepelekea watu kadhaa kuibua hoja ya kutaka Mjadala wa Kitaifa kuhusu mfumo wa elimu.” ,sera ya Elimu ya taifa na Lugha ya kufundishia na kujifunzia


Mimi nadhani ni vema kabla ya kwenda moja kwa moja kwenye mfumo wa elimu hapa nchini ni vema tukarudi nyuma kidogo katika falsafa yetu ya elimu.Katika kipindi hiki kigumu ni lazima tuamue sasa katika ugumu huo kuona ni aina ya falsafa ya elimu na ndipo twende katika mfumo mzima wa elimu.Tunapaswa kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya ufanisi wa taifa letu.Lazima tuwe na mwanzo.Na mwanzo ni “Tafakuri”.Tafakuri kuhusu aina ya falsafa itakayotuongoza na kutuletea ufanisi katika dunia yetu,Ile “Dunia Bora kwa watu wote” tunayoitarajia.


Falsafa ya Elimu ya taifa tunayoitaka,itakayoendana na aina ya taifa tunalolitaka ni moja ya maswali

korofi” yanayonigonga kichwa kila uchao.Ila kama walimu hatuna namna ya kuyakwepa maswali ya aina hii.Ni lazima kama sehemu muhimu ya jamii tujifunze kuwa na utamaduni wa kujiuliza maswali ya aina hii.Tujiulize tukiwa na dhamira ya kuyapatia ufumbuzi na si vinginevyo.


Matharani,tunapoiangalia falsafa yetu ya elimu kwa sasa”Elimu ya kujitegemea” ni vizuri tukarudi nyuma na kusawiri /kuyaelewa mazingira yaliyopelekea kuibuka kwa kwake ambayo ni kutangazwa kwa Azimio la Arusha.1967,pale tulipoamua kufuata siasa ya “Ujamaa na kujitegemea” ambayo imejengeke katika misingi ya Usawa wa Binadamu na kufutwa kwa unyonyaji.


Ili kufanikisha siasa ya ujamaa na kujitegemea,falsafa ya elimu ya kujitegemea ilitangazwa ili kuwajenga Watanzania katika misingi ya kijamaa.Lengo likiwa ni kumkomboa Mtanzania kutokana na Ukoloni mkongwe,kuwafanya watu wawe huru na kuwa na uwezo wa kujitegemea.


Miongo kadhaa sasa tangu Azimio la Zanzibar lilipopitishwa ili kuthibitishwa Arusha kupewa kisogo ilihali bado tunajidai kutekeleza falsafa ile ile iliyotokana na Azimio la Arusha.Falsafa yetu ya elimu katika Dunia ya leo inakosa mantiki kwa sababu mfumo wetu wa elimu haumtayarishi kijana wa kitanzania kuwa na moyo wa kujitolea na wa kizalendo kama ilivyokuwa imekusudiwa na badala yake umeua moyo wa ushirikiano na kuyashawishi maendeleo binafsi.Hii ni kutokana na ukweli kuwa tunaifuata falsafa ya elimu ya kujitegemea kwa nadharia wakati tukitekeleza kwa vitendo falsafa ya elimu ya “Kidhalimu”


Ujenzi wa mfumo mpya wa elimu kulingana na Mabadiliko ya jamii ya sasa na ijayo ni lazima ujiegemeze katika dhamira moja kuu itakayotokana na kuwa na falsafa maridhawa ya Elimu ya Taifa